Ijumaa, 3 Juni 2016

uteketezaji wa familia

Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameshutumu vikali tukio la uteketezaji wa nyumba ya mwakilishi wa wadi ya Menengai Magharibi Lucy Kihumba.
Nyumba pamoja na mali ya mwakilishi wadi huyo iliteketezwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia siku ya Jumanne.
Akizungumza alipozuru eneo la tukio hilo huko Ol-Rongai alipokwenda kuijulia familia hiyo hali na kuipa pole, Gavana Mbugua alitaja kitendo hicho kama kiovu huku akitaka waliotekeleza hatia hiyo kukamatwa haraka iwezekanavyo na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa muujibu wa sheria.
“Kile ambacho nimeona hapa si ajali. Ni jambo lililopangwa vizuri. Ni lazima hatua zote zichukuliwa hukakikisha waliotekeleza ovu huu wamekamatwa,” alisema Mbugua.
Gavana huyo pia ametaka uchunguzi wa haraka ufanywe huku akiwahimiza viongozi wa Kaunti ya Nakuru kwa jumla kujifunza kutokana na tukio hilo na haswaa kuhusiana na swala la kiusalama akisema usalama ni muhimu ikizingatiwa kazi wanayoifanya.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba tukio hili limempata mmoja wetu ili tuweze kuona umuhimu wa usalama wetu. Natoa pole zangu kwa familia hii lakini pia nawahimiza kujipa moyo kwani wako hai, kwa kuwa hakuna maafa yoyote yaliyotokea. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hayo,” alisema Mbugua.
Mbugua alihakikishia familia hiyo kuwa serikali yake ya kaunti itawaunga mkono wakati huu wanapopitia wakati mgumu.
Baadhi ya walioandamana na Gavana Mbugua alipomtembelea mwakilishi huyo wa wadi ni Spika wa bunge la Kaunti ya Nakuru Susan Kihika, Katibu wa kaunti Joseph Motari, Kiongozi wa walio wengi katika bunge la Kaunti ya Nakuru Withuki Njane nazaidi ya wawakilishi wa wadi 50.
Uchunguzi kuhusiana na kisa hicho tayari umeanzishwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni