Jumanne, 7 Juni 2016

Balozi wa Marekani akabidhi ruzuku kwa vikundi vya kijamii


24, Agosti, 2015

Balozi wa Marekani Mark B. Childress akihutubia wawakilishi wa mashirika ya kijamii katika hafla ya kukabidhi ruzuku iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam (Picha: Ubalozi wa Marekani)
Balozi wa Marekani Mark B. Childress akihutubia wawakilishi wa mashirika ya kijamii katika hafla ya kukabidhi ruzuku iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam

Balozi wa Marekani Mark B. Childress akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kijamii baada ya kuwakabidhi ruzuku katika hafla iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam. (Picha: Ubalozi wa Marekani)
Balozi wa Marekani Mark B. Childress akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kijamii baada ya kuwakabidhi ruzuku katika hafla iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.

Hapo tarehe 24 Agosti 2015, Balozi wa Marekani nchini Tanzania alikabidhi ruzuku kwa vikundi na mashirika ya kijamii 14 yanayofanya kazi ya kuboresha maisha ya Watanzania katika hafla iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam. Inatarajiwa kuwa ruzuku hiyo itawanufaisha moja kwa moja zaidi ya watu 5000 katika mikoa 12 humu nchini na itaboresha huduma na fursa katika sekta za maji na usafi wa mazingira, afya, elimu na maendeleo ya kiuchumi.

Ruzuku hizi zinatolewa chini ya programu maalum ya Ubalozi wa Marekani ya kusaidia vikundi na mashirika ya kijamii (Community Grants Program) ambayo hutoa msaada wa moja kwa moja kwa miradi midogo inayolenga kuboresha maisha ya jamii husika kupitia Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii (Ambassador's Special Self-Help Fund) na  Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI (Ambassador's Fund for HIV/AIDS Relief). Mfuko wa Balozi wa kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii hutoa ruzuku za moja kwa moja kwa mashirika na vikundi vya kijamii kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayolenga kunufaisha jamii za vijijini na mijini wakati ambapo Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI hutoa msaada mahsusi kwa jamii zilizoathiriwa zaidi au zilizo katika hatari zaidi ya kuathiriwa na VVU/UKIMWI.

Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii ulianzishwa wakati wa muhula wa kwanza kwa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere. Kwa miaka 50 sasa mfuko huu umesaidia taasisi na vikundi vya kijamii kutoka kila mkoa wa Tanzania ili kuboresha Maisha ya Watanzania kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga shule, kuwezesha upatikanaji wa maji safi, matumizi ya nishati ya jua na uanzishaji wa miradi ya kuongeza kipato. Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI ulianzishwa mwaka 2009 na hadi sasa umetoa ruzuku kwa vikundi vya kijamii 69 nchini Tanzania. Mifuko hii inaendeleza utamaduni wa ushirikiano kati ya raia wa Marekani na Tanzania.

Ruzuku kupitia Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii kwa mwaka 2015 zinatolewa kwa:

Chama Cha Wazazi Wenye Watoto Walemavu Tabora (CHAWAWAWATA) ambacho kitatoa mashine 5 za kutengenezea siagi ya karanga kwa vikundi vitano vya wanawake mkoani Tabora.

Congregation of the Mission litajenga vyoo kwa shule mbili za msingi katika mkoa wa Ruvuma.

Kituo cha Walemavu Iyunga mkoani Mbeya kitatoa vyerehani 23 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ushonaji kwa vijana na watu wenye ulemavu.

Jumuiya ya Maendeleo Jimbo la Ziwani (JUMAJZI) itatumia fedha za ruzuku ili kukamilisha ujenzi wa maktaba ya maabara ya sayansi katika Shule ya Sekondari ya Kwale Mini kisiwani Pemba.

Shule ya Sekondari Kangagani kisiwani Pemba itatumia fedha za ruzuku kumalizia kazi ya kupaua madarasa sita na ofisi mbili.

Karakana ya Walemavu Dodoma (KAWADO) itatoa vitendea kazi na malighafi kwa ajili ya mafunzo ya kutengeneza viti vya magurudumu (wheel chairs) kwa walemavu wapatao 50 mkoani Dodoma.

Kituo cha Bikira Maria (Mary Mother of God Perpetual Help Center) kitatoa vitanda, magodoro, mashuka na mito kwa watu wenye albinism na ulemavu mwingine katika mkoa wa Simiyu.

Tumaini la Maisha Tanzania – Wodi ya Watoto wenye Saratani Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam, watatumia ruzuku itakayotolewa kutafsiri mwongozo wa wazazi/walezi kuhusu namna ya kuwahudumia watoto wenye saratani, watafanyia ukarabati vifaa vya kuzimia moto na vifaa vya kusafishia maji (water filters), kununua vitabu vya shule kwa watoto, DVD player na kompyuta na program ya masuala ya fedha kwa ajili ya idara yake ya fedha.

Kikundi cha Kinamama Sangananu Ukombozi cha Usa River, mkoani Arusha, kitanunua vyerehani vitatu pamoja na vifaa vingine vya ushonaji.

Shirika la Kujenga Uwezo kwa Jamii, cha Njombe (SHIKUJANJO) litatoa vifaa vya maabara kwa Shule ya Sekondari ya Mabatini nkoani Njombe.



Veyula Community Skills Development Organization kitanunua vitendea kazi na vifaa vingine kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wapatao 100 mkoani Dodoma.

Ruzuku kupitia mfuko wa Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI  zinatolewa kwa:

Jipe Moyo - Hunyari Positive watatumia ruzuku itakayotolewa kununulia mbuzi 17 na kujenga mabanda kwa lengo la kuwawezesha watu wanaoishi na UKIMWI mkoani Mara kupata lishe bora.

Rural Women Development Initiative (RUWODI) watatumia ruzuku itakayotolewa kununulia vyerehani 17, samani na mahitaji mengine ili kuweza kutoa mafunzo ya ushonaji kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI na watoto waliokatika mazingira hatarishi katika mkoa wa Pwani.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Bega kwa Bega (ELCT) na Wabia wa Saint Paul Tz watatumia ruzuku kununulia pampu ya maji inayotumia nishati ya jua (solar power pump) na matanki mawili ya maji kwa ajili ya zahanati ya Lukani mkoani Iringa.

Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii na Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na UKIMWI ni sehemu ya programu ya Balozi wa Marekani ya kutoa ruzuku kwa miradi mbalimbali ya kijamii. Kwa maelezo zaidi kuhusu programu hii kufahamu, tafadhali tembelea tovuti ya Ubalozi wa Marekani au wasiliana na Afisa wa Ubalozi Anayeshughulikia Ruzuku kwa anuani ya barua pepe selfhelpd@state.gov au kwa barua kupitia S.L.P 9123, Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni